October 31, 2018

MCHANGANUO WA KUFUGA KUKU WAKIENYEJI

*MAHITAJI*

1- Tetea 10 kwa jogoo 1

2- Banda bora

3- Vyombo vya chakula na maji

4- Chakula bora

5- Madawa na chanzo cha nishati joto na mwanga

6- Elimu na ujuzi wa malezi bora

7- Chombo au chumba cha kutunzia vifaranga

8- Mayai ya kuku wa kisasa/mayai mabovu(ambayo hayakuanguliwa)

9- Madaftari au kitabu cha kutunzia kumbukumbu


*KUKU 10*

1- Wakati wa kuanza mradi wako hakikisha una kuku 10 *(matetea)* wenye umri sawa na hawajawai kutaga hata mara moja.


2- Chagua kuku wenye rangi nzuri kutoka katika familia bora kutegemea malengo ya mradi wako.


3- Mfano kama lengo lako ni kuzalisha kuku wa kienyeji kwajili ya nyama basi chagua mbegu ambayo inakuwa haraka na yenye uzito mkubwa.


4- Au ikiwa lengo ni mayai basi ni vema kuchagua aina ya kuku yenye kukua haraka na kutaga mayai mengi.


5- Ili kupunguza gharama za manunuzi ya kuku na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji ni vema kununua kuku wadogo ambao wametoka tu kuachishwa kulelewa na mama zao.


6- Kuku hawa utawapata kwa bei ya chini, tena watafaa sana maana watakua na umri mmoja pia.


*JOGOO 01*

1- Jogoo mmoja tu anatosha kuwahudumia kuku matetea yote kumi.


2- Hakikisha katika uchaguzi wa jogoo bora lililochangamka, rangi mzuri, upanga umesimama, macho angavu, uzito wa kutosha, rangi nzuri na uwezo mkubwa wa kuzalisha.


3- Ni vema mfugaji akaelewa kwamba kuku wote watakaozalishwa watategemea ubora wa jogoo wake.


4- Uwezo wa kutaga kwa kuku na upatikanaji wa mayai pia hutegemea kwa karibu ubora wa jogoo aliyechaguliwa.


*BANDA BORA*

1- Miongoni mwa mambo mhimu naya kwanza kuzingatiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kama mradi ni maandalizi ya banda bora.


2- Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali.


3- Mfugaji anatakiwa kuandaa banda lenye ukubwa wa mita 10 kwa mita 04.


4- Yani urefu uwe mita 10 na upana upana wa mita 04. Kisha kata vyumba vya mita 2 urefu na upana mita 4 kutoka katika banda lako hivyo utakuwa na jumla ya vyumba vitano vyenye ukubwa unaolingana.


5- Ujenzi uzingatie malighafi na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira husika.


 Mfano katika maeneo ambayo fito zinapatikana kwa urahisi banda linaweza kuandaliwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo.


6- Au sehemu ambayo mabanzi hupatikana kwa urahisi basi banda laweza kujengwa kwa kutumia mabanzi.


7- Vifaa vya kujengea banda vizingatie pia gharama na upatikanaji wake katika eneo husika.


*Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-*

1- *Sakafu*

√Saruji

√udongo

√mbao

√mianzi/fito


*Kuta*

√Fito/mabanzi mbao,

√nguzo mianzi

√udongo,

√matofali,

√mawe

√mabati

√wavu


*Paa*

√Nyasi

√makuti

√majani ya migomba

√mabati/vigae.


*Wigo*

√Matofali

√mbao

√fito/nguzo

√mabanzi/mianzi

√matete, wavu na mabati


*Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-*


*Imara*

1-/Lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.


2- Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.


3- Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.


4- Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala


5- .Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga.


6- Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji.


7- Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa.


8- Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga.


*JINSI YA KUFANYA*

1- Wakuze kuku wako hadi watakapofikia muda wa kutaga.


2- Wakianza kutetea ni kiashiria kwamba wakati wa kutaga umekaribia hivyo andaa viota kwajili ya kutagia.


3- Viota vinapaswa viwe na ukubwa stahiki ili kumwezesha kuku kuyafunika mayai yote vizuri wakati wa kuatamia, viota viwe vinavyozuia mayai kutawanyika, viwe mahali pakavu na safi.


4- Hakikisha kuku wote wanataga katika viota tofauti.


5- Kuku anapotaga mayai matatu unapashwa kuchukua mayai mawili na kumwachia yai moja ili kumfanya aendelee kutaga zaidi.


6- Kuku akifikia yai la kumi na mbili anza kumwachia mayai matatu ili kumwandaa kwa kazi ya kuetamia.


7- Kwa kufanya hivi, kuku atataga mayai 15 au zaidi na ikiwa atataga mayai 15 au chini ya hapo nakushauri utafute mayai mengine ujazilizie ili kufikisha mayai 20 kwa kila kuku.


 *Zingatia kwamba mayai unayoyatoa kwa kila kuku, yanatunzwa sehemu salama, mahali pakavu, pasafi na penye joto la wastani*


8- Kuku wote wanapaswa kuanza kuatamia kwa siku moja. Ili kufanikisha hili inapasa uwe karibu na kuku wako.


9- Kuku mmoja akianza kuatamia mwekee mayai ya kuku wa kisasa au mayai mabovu ya kuku wa kienyeji.


10- Utafanya hivi hadi kuku wako wote watakapoanza kuatamia mayai.


11- Kuweka mayai mabovu au mayai ya kuku yaliyotumika humfanya kuku aendelee kuatamia akijua ni mayai yake.


12- Baada ya kuona kwamba kuku wako wote wapo tayari kwa kuatamia mayai, waandalie banda maalumu kwajili ya kuatamia yani chumba kimoja katika lile banda letu.


13- Ninashauri kwamba chumba kwajili ya kuatamia kiwe chumba cha kwanza au cha mwisho katika mfuatano wa vyumba vya banda lako. Andaa viota bora vya kuatamia, weka mayai 20 kwa kila kiota, ikiwa hayajatimia unaweza kununua kwa wafugaji wengine ili kuifikia idadi yako.


14- Waamishe kuku kutoka wanapotagia na kuwaweka katika chumba ulichokiandaa kwajili ya kuatamia.


15- Ili ufanikiwe katika zoezi hili inafaa lifanyike wakati wa usiku na unafanya katika giza.


16- Mweke kuku katika kila kiota na asubuhi wajikute kila mmoja katika kiota chake.


17- Wahudumie kwa chakula na maji ya kutosha. Wakati wa usiku waongezee joto la ziada kwa kuweka jiko au ndoo ya chuma yenye chengachenga za mkaa au kama una umeme weka taa za joto.


28- Baada ya siku 21-25 kuku wako wataanza kuangua vifaranga.


29- Huu ndio wakati unaotakiwa kuwa karibu sana na kuku wako kuliko wakati wote.


30- Watenge vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa; waweke katika chumba chao maalumu mbali na kuku.


31- Kama chumba cha kuatamia kilikuwa cha kwanza basi vifaranga wawe chumba cha mwisho n.k


32- Ukishawatenga vifaranga mbali na matetea wako, wawekee tena mayai mengine 20 kila tetea, mayai ambayo utayanunua kwa wafigaji wenzako.


33- Hakikisha kuku waliotaga hayo mayai ni wazuri, hawana magonjwa na wanauzito/ukubwa unaofaa.


34- Mayai yote yakaguliwe vizuri ili kujua kwamba yameharibika, yana nyufa au mabovu. Kabla ya kuweka mayai mengine hakikisha chumba chako ni kisafi na viota vimesafishwa, havina wadudu na uchafu wowote.


35- Kuku wako bila kujijua wataanza kuetamia upya mayai uliowawekea.


36- Ukiwawekea mayai rudia mzunguko kama nilivyokwambia awali.


37- Baada ya siku 21 hadi 25 tena utapata vifaranga wako wengine tena. Fuata kila hatua kama nilivyokwambia hapo awali. Lakini kwa awamu hii nashauri waache matetea wako wapumzike wala usiwapatie mayai mengine tena.


*JINSI YA KULEA VIFARANGA*

1- Ikikaribia siku ya 20 tangu ulipowawekea matetea wako mayai katika chumba cha kuetamia, andaa chumba kwa ajili ya kulea vifaranga


2- Safisha kwa kuondoa uchafu na wadudu wote.


3- Washa taa ya joto au weka chombo cha kutoa joto katika chumba cha vifaranga nusu saa kabla huja anza kuingiza vifaranga wako. Weka pia chakula na maji ya kutosha katika vyombo vyenye umbile na ukubwa utakaowawezesha vifaranga kuvitumia


4- Tandaza magazeti, maboksi, makaratasi n.k katika sakafu ya chumba hicho. Hakikisha vifaranga wako hawajikusanyi sehemu moja maana wakifanya hivyo wengi wao watakufa ili ufanikiwe katika jambo hili, banda lako liwe la mduara katika kona zake.


5- Weka joto la kutosha. Joto la kutosha ni lile linalowafanya vifaranga watawanyike chini ya chanzo cha joto wakati kama joto limezidi vifaranga kukimbia mbali na chanzo cha joto na ikiwa joto halitoshi vifaranga hujukusanya chini ya chanzo cha joto.


6- Baada ya siku 3 utawapatia chanjo ya Gumboro na siku 7 wapatie chanjo ya New Castle, utarudia tena kuwapa chanjo hii baada ya mwezi mmoja kisha utafanya hivi kila baada ya miezi mitatu mitatu.


*MAPATO YA MRADI WAKO*

1- Katika uzazi wa kwanza utapata vifaranga 150 kwa wastani wa vifaranga 15 kwa kila kuku. Tuseme haujazingatia kanuni za ufugaji za makala hii ukapata vifaranga 100 yani wastani wa vifaranga 10 kwa kila kuku. Kisha baadaye wakakua wakafa kuku 50 yani watano kwa kila kuku utakuwa na jumla ya kuku 50.


2- Baada ya wiki 3 utapata tena kuku tufanye kwa mahesabu kama hayo hapo juu kwa hasara utakuwa na kuku wengine 50, na kufanya jumla ya kuku 100. Ikiwa kuku wako baada ya uzao wa pili uliwapumzisha kwa miezi miwili basi mwezi wa 3 utapata tena kuku vifaranga 100 na wiki 3 baadaye utapata wengine 100. Kwa mahesabu kama hayo awali wakikuwa utakuwa na kuku wengine 100 ambao watakuwa.


3- Baada ya miezi 6 utakuwa na kuku wakubwa wa uzao wa kwanza 50, uzao wa pili kuku 50 na utakuwa na kuku wenye umri wa miezi mitatu 50 wa uzao wa 3 na kuku wengine 50 wa uzao wa 4.


4- Katika kuku 100 wa uzao wa kwanza na pili, tufanye kuku 50 wawe matetea ukijumlisha na kuku 10 ulioanza nao mradi utakuwa na matetea 60. Ikiwa kila tetea atatotoa vifaranga 10 na vikakua vitano tu, mwishoni utakuwa na kuku 300 na baada ya miezi mitatu kuku wengine 900 toka katika kutoka kwa uzao wa kwanza, wapili na watatu.


5- Hivyo mwaka wa pili utafunga na kuku si chini ya 1,200/= wanaotaga mayai.


6- Ukiuza majogoo yote 1,200/= kwa bei ya 8,000/= ili upate pesa ya kujenga miundombinu bora maana sasa utakuwa na kuku wengi wanaoendelea kuzaliana kwa kasi utapata pesa kiasi cha *TZS 7,200,000/=*


Sasa ongeza kuku wako wa kutaga hadi wafikie kuku 4,000 maana sasa utakuwa na pesa za kutosha kuendesha mradi wako.


7- Sasa ukiwa na kuku *4000* wa kienyeji wa kutaga mayai, ikiwa kuku *3000* tu watataga ukauza yai moja kwa bei ya haraka haraka ya *TZS 250* tu, utapata *TZS 750,000/=* kwa siku ambayo sawa na TZS *22,500,000/=* kwa mwezi na *TZS 270,000,000/=* kwa mwaka sawa sawa na *128,572 USD*. Kumbuka mwamba makadilio haya niya chini sana. Ukifata kanuni zote kwa makini na maombi huku ukimtanguliza Mungu utafikia hata TZS *500,000,000/=* kwa mwaka.


8- Kumbuka unapofanikiwa kupata mapato ya kila aina, umtolee *Mungu zaka(x10%)* ya mapato yako, pia ukatoe sadaka ambayo ni kubwa kuliko zaka na uwasaidie masikini na wahitaji.


9- Tunza kumbukumbu zako zote za fedha katika daftari maalumu kuhusu mapato na matumizi ya mradi wako. Pia hali ya kuku wako kuhusu tarehe za chanjo ya mwisho, siku walipoanza kuatamia, magonjwa yanayowasumbua mara kwa mara.

October 26, 2018

Kutuhusu ebusol

MILK SHAKE YA EMBE

MAHITAJI

1-  Maembe makubwa 3

2- 1/2 kijiko kidogo cha chai unga wa hiriki 

3- Cardamom powder (weka kidogo kidogo kulingana na ladha)

4- Sukari *vijiko 2* vya chakula

5- *240 gram* ya maziwa ya maji

6- Vipande vya barafu

*(Ice cubes)*

7- Kijiko 1 cha chakula cha vanilla ice cream

*Unaweza tumia maembe yaliyogandishwa katika friji*


Menya maembe kisha weka katika Brenda


Weka maziwa ya maji na cardamom powder. Washa blenda yako kwa kasi ndogo ili kusaidia isage pole pole ukipata mapovu toa kwa kijiko.


Kisha weka barafu na endelea kusaga ipondeke kabisa na barafu.


Kisha ongeza sukari na jitaidi kulamba/kuonja uweze pata ladha unayoitaka.


Baada ya hapo kinywaji kitakuwa tayari kwaajili ya kunywa/kuuza pia unaweza weka ice cream wakati wa matumizi

October 25, 2018

JINSI YA KUTENGENEZA EGG CHOPS ZA NYAMA NA UNGA WA MCHELE

Mahitaji

1- Mayai 8 makubwa au 10 madogo

2- Nusu kilo ya nyama =na gm 500 na nyama hii iwe ya kusaga

3- Kitunguu1cha wastani

4- Kijiko 1 cha chakula cha  kitunguu saumu na tangawizi

5- Binzari manjao kijiko 1 cha chai au nusu inatokana na inavyokolea maana manjano nyingine huwa Kali sana hivyo unahitajika kuwa mwangalifu.

6- Kijiko 1 cha chai garam masala powder

7- Robo *(¼)* kikombe majani ya kotimiri/ giligilani

8- Chumvi kwa kuonja

9- Nusu *(½)* kikombe unga wa mchele

10- Mafuta ya kukaangia


*Maelekezo*

Weka mayai kwenye sufuria ukiwa umeyaosha vizuri na ubandike jikoni jiko likiwa na moto wa wastani chemsha mayai yaive kama unavyopenda. 


Wakati mayai yanachemka, andaa viungo vingine; katakata majani ya kotimiri na kitunguu vipande vodogovidogo sana


Katika bakuli kubwa; weka nyama, kitunguu, majani ya kotimiri, kitunguu saumu na tangawizi, bizari ya manjano, pilipili ya unga na garam masala. 


Vunja yai moja uongeze kwenye mchanganyiko. 


Changanya vizuri, weka na chumvi kwa kuonja


Gawanya mchanganyiko kwenye madonge 6 hadi 8 yaliyolingana (inategemea na ukubwa wa mayai). Menya na mayai, weka pembeni


Funika kila yai na donge moja ya nyama. Hakikisha yai linakuwa katikati na limefunikwa vizuri na nyama.


Sawazisha vizuri kwa juu kisha paka unga wa mchele kwenye madonge ya nyama kwa juu, hakikisha kila sehemu imefunikwa vizuri


Chemsha mafuta kwenye kikaangio katika moto wa wastani. 


Wakati mafuta yanachemka, piga yai moja lililobakia. 


Chovya kila egg chop kwenye yai, tingisha kidogo ili yai lililozidi litoke kabla ya kuweka kwenye mafuta


Kaanga mpaka ziwe na rangi ya kahawia


Hamishia egg chops zilizoiva kwenye sahani iliyowekwa tissues za jikoni au chujio la bati ili mafuta yote yachuje kishaa Itakuwa tayari kwa biashara

October 23, 2018

JINSI YA KUPIKA WALI WA RANGI TATU

MAHITAJI

WALI WA MANJANO

1- Mchele wa basmati kikombe 1 cha chai

2- Mafuta ya kupikia kijiko1 ½ 

Nyanya 2 zilizomenywa na kukatwakatwa

3- Karoti 3 zilizochemshwa na kuiva

4- Unga wa binzari 1/4 kijiko

Chumvi kiasi 

5- Kwa wali wa mweupe

6- Mchele wa basmati kikombe 1 cha chai

7- Mafuta ya kupikia kijiko1 ½ 

8- Tui la nazi kikombe 1

9- Unga wa hiliki Kijiko 11/2 chachai


*WALI WA KIJANI*

*MAHITAJI*

1- Mchele wa basmati kikombe 1 cha chai

2- Mafuta ya kupikia kijiko 1 ½ 

3- Chumvi kiasi

4- Vitunguu maji 2

5- Kitunguu saumu kilichopondwa 1

6- Tangawizi iliyopondwa 1

7- Nazi iliyosagwa vijiko 2

8- Majani 8 hadi 10 ya mnanaa

9- Majani ya giligilani kikombe kimoja

10- Pilipili manga kijiko 1

11- Garam masala kijiko 1 cha chai

12- Namna ya kuandaa

13- Unatakiwa kupika wali walo katika sufuria tatu tofauti. Kwa 


*WALI MWEUPE*

1- Wali mweupe unatakiwa kupika kama ilivyozoeleka huku ukiongeza hiliki kama kiungo chako.


2- Unachotakiwa kufanya ni kuosha mchele wako.


3- Kisha injika tui jikoni weka chumvi na baadaye hiliki.


4- Hakikisha maji uliyoinjika yana uwezo wa kuivisha wali wako.


5- Baada ya kuiva palia na weka pembeni.


*KWA WALI WA RANGI YA CHUNGWA*

1- Anza kwa kupika wali wa mafuta. Kwa kuosha mchele na kuuchemsha kwa kiwango cha maji ya kutosha kuivisha.


2- Hakikisha unaweka chumvi ili kuufanya wali wako kuwa na ladha.


3- Chukua karoti na nyanya saga pamoja.


4- Kisha kaanga binzari na changanya na mchanganyiko wa nyanya na karoti.


5- Chukua wali wako uliokwishawiva na changanya katika mchanganyiko wako huo.


6- Wali wote utakuwa wa rangi ya chungwa.


*WALI WA KIJANI*

1- Kwa wali wa kijani , anza kwa kupika wali wenyewe kama nilivyoelekeza hapo juu.Kisha chukua kitunguu maji, saumu, tangawizi nazi , majani ya mnanaa,majani ya giligilani,hoho, pilipili manga na kisha saga kwenye machine ya kusagia.


2- Chukua mafuta ya kupikia weka jikoni, na kaanga garam masala na baadaye weka mchangayiko wako wa kijani kwenye sufuria hiyo iliyoko jikoni.


3- Endelea kukaanga hadi viive kabisa.


4- Ipua na changanya na wali wako. Utapata wali wa kijani.

Baada ya hapo pakua. Na weka kwenye bakuli lenye muundo unaopendelea.


5- Anza kwa kuweka rangi yeyote kati ya hizo ulizopika. Panga vizuri kwa kufuata mpangilio maalum unaweza kuanza na rangi ya machungwa, nyeupe na kijani ikaja mwisho au kinyume chake.


6- Pamba wali wako kwa kuweka jani dogo la giligilani na kipande cha karoti.

Chakula choko kipo tayari kwa kuliwa

UTENGENEZAJI WA TAMBI ZA DENGU

MAHITAJI

1.    Unga wa dengu ½ kilo


2.    Binzari nyembamba ½ kijiko cha mezani


3.    Unga wa pilipili manga kijiko 1 cha chai


4.    Unga wa mchele ¼ kilo


5.    Chumvi kiasi


6.    Mafuta ya alizeti ½ lita


7.    Baking powder


*JINSI YA KUTENGENEZA*

1- Changanya unga wa mchele pamoja na ule wa dengu. Kisha chukua nyunyuzia baking powder na baadaye chumvi


2- Weka unga wa binzari nyembamba na pilipili manga.


3- Changaya vizuri na kisha weka maji kidogo kidogo huku ukukanda hadi liwe donge gumu kama unavyofanya kwenye maandazi.


4- Baada ya hapo weka donge lako pembeni na funika. Acha likae kwa muda wa nusu saa hadi saa moja.


5- Baada ya hapo chukua karai la mafuta weka jikoni acha hadi mafuta yapate moto kabisa. Kisha chukua mashine ya kupikia tambi na weka donge lako. Kandamiza taratibu huku ukiruhusu minyororo ya tambi kuingia kwenye mafuta yaliyo jikoni.


6- Weka kiasi kiasi huku ukikaanga. Acha mpaka zitakapokuwa zimeiva na kukauka vizuri. Ipua na weka pembeni.


7- Weka kwenye sahani safi na kavu.Tambi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.


8- Tafuta fingushio vizuri funga kisha peleka sokoni 

October 22, 2018

JINSI YAKUTENGENEZA MAANDAZI YA MAYAI NA MAZIWA

Mahitaji

1- Unga wa ngano ½ kilo

2- Sukari 200g (kikombe kimoja cha chai)

3- Chumvi ½ kijiko kidogo (cha chai )

4- Hamira kijiko 1 kidogo

5- Yai 1

6- Maziwa ya unga vijiko 2 vikubwa

7- Butter kijiko 1 kikubwa

8- Iliki kijiko1 kidogo

9- Maji ya uvuguvugu ya kukandia

10- Mafuta ya kuchomea lita 1

11- Kibao cha kusukumia unga wa ngano

12- Sinia au ubao ulionyooka


*Maelekezo*

1- Weka unga kwenye bakuli kisha ongeza sukari, chumvi, yai, maziwa ya unga, butter na hiliki. 

2- Changanya viambato mpaka mchanganyiko uwe sawia.

3- Ongeza maji ya uvuguvugu kiasi kwenye mchanganyiko na uanze kukanda. 

4- Ni vizuri kukanda mchanyiko huu kwa muda wa dakika 15 ili kuhakikisha donge lote la unga limelainika vizuri.

5- Gawanya unga uliokwandwa katika madonge manne (4) tofauti.

6- Weka unga wa ngano kidogo katika kibao cha kusukumia na uanze kusukuma donge moja katika shape ya chapati. 

7- Katika kusukuma, hakikisha unga wako uko wa wastani – siyo mwembamba sana wala mnene.

8- Ukimaliza kusukuma kata unga kutokana na umbo upendalo kupika maandazi na uyatandaze katika ubao au sinia lililonyooka. 

9- Hakikisha sinia au ubao umenyunyuziwa unga wa ngano ili kuzuia unga utakaoweka usingandie.

10- Rudia hiyo hatua kwa madonge yote yaliyobakia.

11- Ukimaliza kuandaa maandazi yako, weka maandazi yako katika sehemu iliyokuwa na joto ili yaweze kuumuka. 

12- Hii inaweza kuchukua hadi masaa 3 ili hamira kuumua vizuri unga wako.

13- Unga ukishaumuka, bandika sufuria, au kikaangio pamoja na mafuta jikoni

14 Hakikisha mafuta ni mengi ili kuwezesha maandazi kuiva vizuri.

15- Mafuta yakishachemka tumbukiza mandazi. 

16- Acha maandazi kwenye mafuta mpaka yabadilike rangi na kuwa ya brown.

17- Maandazi yakishaiva, ipua na weka kwenye chujio ili kukausha mafuta. Rudia hatua hizi kwa maandazi yote yaliyobaki.

18- Subiri yapoe na yako tayari kuliwa/kuuza