July 28, 2018

Kilimo Bora na rahisi Cha karoti

UTANGULIZI
Karoti ni zao la mbogamboga ambalo ni zao mzizi, kwa kawaida hupatikana katika rangi ya machungwa, zambarau, nyeusi, nyekundu, nyeupe na njano. Karoti za sasa zimetokeza kutokana na karoti pori, Daucus carota. Karoti hutumika sana kwaajili ya kuongeza radha kama kiungo kwenye mboga au kwenye kachumbari na pia zinafaida kubwa katika mwili kwa kukupatia vitamin A na C pamoja na madini ya chuma.

ASILI YAKE 
Asili ya zao hili ni Persia – Ulaya na kusini magharibi mwa Asia. Kwa Tanzania zao hili hulimwa hasa mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Arusha, Kagera na Kilimanjaro.

HALI YA HEWA & UDONGO
Karoti zinahitaji hali isiyokuwa na joto sana, wala baridi sana, kati ya nyuzi za degree 15 mpaka 27 za sentigredi. Kama ukanda wa pwani una joto kali, inatakiwa karoti zilimwa miezi ya majira ya baridi, karoti zinazotoka mazingira ya baridi huwa na radha nzuri pamoja na harufu nzuri. Udongo wa kichanga chepesi na tifutifu ndio unafaa katika kilimo cha karoti, udongo wa mfinyanzi na udongo mzito hudumaza mazao.

UTAYALISHAJI WA SHAMBA
Karoti zinahitaji Shamba la Karoti lilimwe kwa trekta, kwa ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45. Mkulima anatakiwa kuandaa matuta yenye mwinuko wa kimo cha sentimita 28 – 40 kwenye shamba, na upana wa mita 1, pia mita 1.5 umbali wa tuta moja hadi lingine. Kwa maandalizi mazuri tengeneza mifereji midogo ya kusiha mbegu za karoti yenye umbali wa sentimita 15- 20, mifereji minne kwa tuta.

UTAYALISHAJI WA MBEGU
Jinsi ya kujua mbegu nzurizenye uwezo wa kukua bila wasiwasi. Mbegu zenye uwezo wa kuota hutoa harufu kali unapozifikicha. Zilizopoteza uwezo wa kuota huwa hazitoi harufu yoyote. Ili mbegu ziote haraka ziloweke katika maji kwa muda wa saa 24. Baada ya hapo changanya mbegu hizo na mchanga, kwa kiasi kinacholingana ili kupata mtawanyiko mzuri wa mbegu wakati wa kupanda/kusia.

UPANDAJI
Inahitajika uoteshe kwenye kitalu ndipo uhamishie shambani.
Weka mbegu katika chupa ya milimita 100 na toboa kidogo mfuniko, baada ya hapo Sia mbegu katika mifereji ya kupandia kwa kutikisa chupa yenye mbegu, ndipo, Funika mbegu kwa kutumia mboji au mchanga, ukimaliza Nyunyiza maji ya kutosha, Funika tuta na plastiki nyeusi, hatua nyingine Kandamiza plastiki kwa pembeni na kwa mabonge ya udongo ili isipeperushwe na upepo. Mbegu huota baada ya siku 3-5 kutegemea na hali ya hewa. Inakupasa kukagua shamba mara tatu kwa siku. Baadaye Ondoa plastiki mara moja pindi utakapoona mbegu moja tu iliyoota. Usicheleweshe kuondoa plastiki husababisha miche inayoota kufa kwa kuunguzwa na joto lililo katika plastiki. Hapo tayari kwa kupanda shambani.

Upandaji wa moja kwa moja shambani katika matuta au sesa.
Kiasi cha kilo 8 za mbegu kinatosha kupandwa kwenye Hekta moja.

MBOLEA
Weka mbolea aina za asili (samadi au mboji) mwanzoni, ila kama haukutumia mbolea ya samadi au mboji, weka mbolea ya S/A kilogramu 100 kwa hekta kama haukutumia mbolea za asili, kama ulitumia mbolea za asili basi weka kilogramu 50 kwa hekta. kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda. Matumizi ya mbolea za maji yafanyike kila baada ya wiki mbili kutegemea na mahitaji

UPALILIAJI & UNYEVU 
Ili kupata mavuno mengi palilia shamba mara kwa mara ili kuhakikisha shamba halina magugu na nyasi kwa kung’olea kwa mkono, jembe na mangineyo, na kwenye udongo hakikisha kuna unyevu wa kutosha kama sio kipindi cha mvua inatakiwa umwagilie shamba lako kwa wiki mara mbili.

MAGONJWA & WADUDU
MAGONJWA:

  • Madoajani (Leaf Spot):
    Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka.

Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane-M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil.

  • Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot).
    Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi namajani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.

Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
– Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
– Nyunyuzia dawa za ukungu kama vile Dithane M- 45, Blitox, Topsin – M 70% na Ridomil.

  • Madoa Meusi (Black Leaf Spot):
    Huu pia ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia majani na mizizi. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano ambayo baadaye hubadilika na kuwa kahawia. Mizizi huwa na madoa meusi yaliyodidimia. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu, kubadilisha mazao na kuepuka kujeruhi karoti wakati wa kupalilia, kuvuna au kusafirisha.

WADUDU:

  • Minyoo Fundo:
    Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao yajamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unawezakupandamazao ambayo bayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.
  • Imi wa Karoti:
    Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa kama vile Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.
  • Karoti Kuwa na Mizizi Mingi (Folking);
    Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.

UVUNAJI
Karoti hukomaa baada ya wiki 11 mpaka 13 kutoka mda ilipokuwa imepandwa kulingana na hali ya hewa ya eneo ilipolimwa, tani 15 hadi 25 za karoti huvuna katika hekta moja.

SOKO
Karoti inatumika sana na watu mbalimbali, tafuta soko pale unapoona karoti zako zimekaribia kukomaa. Ulizia wanunuzi ni bei gani wataweza kuchukua pia kiasi gani watachukua.

 ebusol.blogspot.com

No comments:

Post a Comment