July 31, 2018

Tujifunze kuhusu kilimo hifadhi

TUJIFUNZE MBINU ZA KISASA ZA KILIMO, LEO TUTAANGALIA KILIMO HIFADHI JAPO KWA UFUPI*_. 

        Katika mfumo wa uchumi wa soko huria, mkulima wa Tanzania hana budi kushindana kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwa gharama ndogo. Inampasa kila mzalishaji kutafuta na kutumia mbinu na maarifa zaidi katika uzalishaji.


        Uchumi wa soko huria umesababisha ongezeko kubwa la gharama za mbolea za viwandani, zana, madawa ya kuulia wadudu pamoja mbegu bora. Katika hali hii ni wazi wakulima ( hasa wadogo wadogo ) hawataweza kumudu ushindani iwapo wataendelea kutumia pembejeo za viwandani.


        Uharibifu wa mazingira ( mmomonyoko wa ardhi, mgandamano wa udongo au udomgongo mfu ) unachangiwa na ongezeko la watu pamoja na gharama kubwa ya zana na pembejeo.      

          Tunalazimika kubadilisha mtazamo wetu juu ya mazingira na mfumo sahihi/endelevu wa Kilimo. Zipo njia za asili za kurutubisha udongo na vilevile Kilimo cha jadi cha kutunza mazingira.


       Wakulima wanashauriwa kupunguza utegemezi wa mbolea za viwandani kwa kujitengenezea mbolea yao wenyewe mashambani kwa kupanda na kufunika ardhi kwa mimea ya mikunde.


MATANDAZO.


       Matandazo ni mimea hai au mabaki inayopandwa kwa madhumuni ya kufunika udongo mwaka mzima.


       Kanuni ya kufunika udongo kwa mimea jamii ya mikunde, nyasi na mingineyo ndiyo muhimu zaidi na ya msingi kuliko zote.


         Mizizi ya matandazo ina uwezo wa kutindua na kulainisha udongo kwa kiwango kikubwa zaidi ya majembe tunayokatulia. Kilimo cha matandazo kinaondoa ulazima wa kukatua.


KUPANDA BILA KULIMA.


         Inawezekana kupanda kwenye matandazo bila kuyalima kwa kutumia zana maalum. Hizi ni pamoja na Mwuo ( Dibbler ), Jembe la mkono, Kipanzi mkono ( Jab Planter), Kipanzi komoleo matandazo ( Direct seeder ).


KANUNI ZA KILIMO HIFADHI MATANDAZO.


- Funika udongo wakati wote kwa mimea hai au mabaki yake.


- Usichome moto, usihamishe mabaki ya mazao, usichungie mifugo holela.


- Usilime/uaikatue udongo.


- Panda kwa kukomelea kwa zana maalum.


- Kilimo cha mzunguko. 


MKUNDE > Nyasi > Mikunde Miti > Nyasi.



HATUA ZA KILIMO HIFADHI.


1. Andaa shamba.


* Punguza uchachu wa udongo kama upo kwa Mbolea ya Minjingu, Chokaa au mmea uitwao Lupins.


* Tindua au katua kina kirefu kuondoa Mgandamano wa udongo kama upo.


* Panda Matandazo yasiyooza haraka na yenye mazap au mabaki mengi. Matandazo yanaqeza kupandwa kwa mfumo wa Kilala bora, Mchanganyiko au Kupokezana.


2. Fyeka na laza matandazo kwa Nyengo, Gogo au Kisu Kidekuzi ( Chopping knife roller ) juma 1-2 kabla ya kupanda zao kuu.


3. Pulizia dawa ya kuua wadudu ( kama ni lazima ).


4. Panda kwenye Matandazo kwa Kipanzi maalum. Weka mbolea ya asili ya kupandia.


5. Palilia magugu nachache yatakayoota kwa kung'olea au kupiga dawa ya magugu.


6. Rutubisha kwa kuongeza kiwango cha mbolea za viwandani ( kwa mwaka wa kwanza ). Dhibiti magonjwa/wadudu hasa kwa dawa za asili.


7. Kwa msimu unaofuata, rudia mzunguko kwa kilimo cha mzunguko wa mazao.


MANUFAA YA KILIMO HIFADHI.


i. Kuongeza mboji na rutuba ya udongo. Hatimaye mahitaji ya mbolea za viwandani hupungua.


ii. Kupunguza mahitaji ya nguvu kazi na muda kwa hadi 60%. Hii inatokana na kutohitajika kukatua na haro.


iii. Kuongeza kiwango cha mvua kupenya kwenye ardhi na udongo kutunza unyevunyevu. Athari za vipindi vya ukame au mvua kupita kiasi ni ndogo zaidi katika kilimo cha matandazo.


iv. Kupunguza mmomomonyoko wa udongo. Matone ya mvua hukingwa yasidondoke kwenye udongo n kuusambaratisha. Uchafuzi wa maji katika mito hupungua.


v. Kupunguza gharama za uzalishaji mazao na kuongeza faida. Baadhi ya Matandazo ( Mucuna, Marejea, Desmodium, Vetch ) yana uwezo wa kudhibiti magugu sugu kama ndago.


vi. Kupunguza uchakavu wa zana, mitambo na mafuta kwenye kilimo.


vii. Kutindua na kulainisha ardhi iliyo gandamana. Mizizi ya baadhi ya mimea ya matandazo ( Mbaazi, Fiwi, Nyonyo, Utupa, Marejea pori ) inaweza kwenda chini hadi futi nne.


CHANGAMOTO ZA KILIMO HIFADHI.


. Ni shida kuwashawishi wakulima, wataalam wa ugani, na hata watafiti kubadili mtazamo na kukubali Kilimo Hifadhi.


. Inahitaji kiwango cha juu cha nidhamu na usimamizi wa kilimo.


. Kuzuia uchungaji holela wa mifugo.


. Kuzuia utayarishaji wa mashamba kwa kuchoma moto.


. Matandazo ni makazi salama ya Panya na Nyoka.


Kwa hiyo ndugu zangu wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo, ni vema kuweza kubadili mawazo na mtazamo wa kifikra katika kuongeza kipato kwa gharama nafuu.

Jinsi kupika maandazi ya nazi

Malighafi

1. Unga wa ngano kilo 1

2. Tui la kwanza la nazi 1/2lita

3. Amira vijiko 2 vya chakula

4. Sukari vijiko 12 vya chakula 

5. Chumvi kijiko 1 cha chakula

6. Hiriki

7. Mafuta ya kupikia

Hatua: Jinsi ya kutengeneza

1. Weka unga kwenye chombo cha kukandia.changanya amira na maji,saga sukari na 

chumvi kwa pamoja kisha changanya vyote kwenye unga wa ngano 

2. Unaweza tia hiriki kama unapenda

3. Anza kukanda unga kwa tui la nazi polepole upate manda.kata manda yako peleka 

kwenye kibao kusukumia na usukume hadi upate unene wa kidole kisha kata umbo la 

maandazi upendavyo kisha peleka sehemu ya wazi na uanike kwa dakika 15

4. Kanga maandazi yako vizuri yasiungulie.tumia moto wa wastani.

Zijue faida za kufuga kuku wa asili

Chakula – nyama ya kuku na mayai hutumika kama chakula muhimu cha wanadamu, chenye 

protini. 

Chanzo cha kipato – mkulima hupata fedha akiuza kuku au mayai.

Chanzo cha ajira – ufugaji wa kuku hutoa ajira kwa jamii.

Kuku hutumika kwenye shughuli za ndoa kama vile kutoa mahari na pia ni kitoweo muhimu 

katika sherehe hizo.

Gharama nafuu za kuanzisha na kuendesha mradi huu.

Ni kitoweo rahisi na chepesi kwa wageni kuliko wanyama wakubwa kama ng’ombe au mbuzi.

Ni kitoweo kisichohitaji hifadhi, hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika.

Kuku na mayai hutumika kwa tiba za asili.

Jogoo hutumika kama saa anapowika nyakati za alfajiri na majira mengine ya siku.

Hutuhabarisha iwapo kiumbe kigeni au cha hatari kwa mlio maalum wa kuashiria hatari.

Mbolea – kinyesi cha kuku kinaweza kutumika katika kurutubisha mashamba ya mazao na 

mabwawa ya samaki.

Kuendeleza kizazi cha kuku wa asili hapa nchini.

Soko lipo la uhakika, ukilinganisha na kuku wa kisasa kwani nyama na mayai yake hupendwa 

zaidi na walaji.

Manyoya ya kuku hutumika kama mapambo, pia huweza kutumiaka kutengenezea mito ya 

kulalia na kukalia.

Shughuli za utafiti – kuku wanatumika katika tafiti nyingi za baiolojia, kama kutambua mambo ya 

lishe.

Shughuli za viwandani:

Mayai yenye mbegu ya jogoo hutumika katika kutengeneza dawa za chanjo.

Magamba ya mayai yanaweza kutumika katika utengenezaji wa vyakula vya wanyama.

Kiini cha njano cha mayai kinaweza kutumika kutengeneza mafuta ya kuoshea nywele 

(shampoo).


Kilimo Bora na rahisi Cha Tikiti maji


UTANGULIZI
Matikiti maji hulimwa kama zao la biashara katika sehemu nyingi duniani zenye hali ya hewa ya joto la wastani. Zao hili lina wapatia watu shughuli za kufanya na hivyo kuwapatia kipato kuanzia kwenye nyanja za uzalishaji hadi kwenye matumizi. Matikiti maji ni mojawapo ya jamii aina ya matunda au mbogaboga inayotambaa. Mimea hii inapatikana katika kundi linalojumuisha mimea mingine kama kama matango,maboga na maskwash. Zao la tikiti maji ni mojawapo ya zao ambalo lina faida kubwa sana ukilinganisha na mazao mengine kwa muda mfupi.

Katika shamba la ukubwa wa shamba la ekali moja(1.acre) lililoandaliwa vizuri, kupandwa na kuhudumiwa vizuri mkulima ana uwezo wa kuvuna kiasi cha TANI 15-36, ambacho kitamsaidia kupata fedha zitakazo msaidia katika mahitaji yake mbalimbali na kuondokana na Umasikini.

HALI YA HEWA
Mimea hii husitawi katika maeneo yenye joto la wasitani yaani haihimili hali ya joto kali sana,baridi kali, mvua nyingi na udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu. Matikiti hukua vizuri katika maeneo yenye joto la wastani wa nyuzi kati ya 21-30 sentigradi. Iwapo mitikiti itapandwa katika maeneo yenye joto chini ya nyuzi 15 za sentigrade huchelewa kuota
Mvua : kwa upande wa mvua matikiti yanahitaji kiasi cha mvua kati ya millimita 400-600 kwa msimu. Mvua nyingi husababisha uwepo wa magonjwa ya fungusi na bakiteria ambayo huathili mavuno.

Hali ya Udongo
Huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile vile haihitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa. Hali ya udongo kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile vile wa kuhimili kwenye udongo wenye pH 5.0

MAENEO YANAYOFAA KWA KILIMO CHA MATIKITI MAJI TANZANIA.
Kwa upande wa Tanzania Inastawi vizuri kwenye ukanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM,Tanga, Morogoro, Mtwara, lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi wa tatu mpaka wa tisa.

UANDAAJI WA SHAMBA
Kabla ya kupandikiza udongo utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa.Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingne ambayo inaweza kuwa ni chanzo cha magonja.

UPANDAJI
Katika shamba la ukubwa wa hecta moja kiasi cha kilo 3-4 cha mbegu kinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila shimo. Usipande katika kitalu kwasababu miche ya mitikiti huwa ni dhaifu sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu hivyo kupelekea kufa kwa miche hiyo. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 - 2 kutoka mstari hadi mstari. Zingatia kutokutumia mbegu za tikiti uliloninua kwasababu linaweza kuwa ni chotara (Hybrid) ambayo hupelekea kushusha kiasi na ubora wa matikiti yatakayo zaliwa kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2)

UPUNGUZAJI WA MIMEA
Mimea ya michikichi huanza kuota, baada ya kama wiki 2. Hivyo katika Mbegu mbili ulizopanda kata moja na uache ule mche wenye afya zaidi ndio uendelee kukua.

Aangalizo using’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki. Vilevile unaweza kupandishia udongo kwenye mashina ili kusaaidia kupunguza maji kutuama kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza rutuba.

Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea matikiti waya ya kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito wa matunda.

Wakati mimea inapo anza kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe (kuielekezea ) kwenye waya na kuifungia.

MATANDAZO (MULCHES 
Matandazo ina maana ya kutumia nyasi na mabaki ya mimea mingne kufunika aridhi. Baada ya miche kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu vile viile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

UWEKAJI WA MBOLEA
Mbolea za viwandani aina ya NPK au mbolea zenye nitrogen kiasi cha gram 10 hadi 20 ziwekwe wakati mimea ikiwa ni midogo mpaka pale maua ya kike yatakapoanza kuonekana. Vilevile samadi inaweza kuwekwa wakati mimea ikiwa midogo. Baada ya mimea kutengeneza matunda weka mbolea aina ya urea na potassium hadi mara 2 au 3 kwa wiki mpaka matunda yatakapokomaa.

UMWAGILIAJI
Shamba linatakiwa limwagiliwe mara kwa mara wakati mvua zinapokosekana au wakati wa mvua chache. Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni katika kipindi cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya kuvuna. Iwapo kutakuwa na ukosefu wa maji kutasababisha kutengenezwa kwa matunda ambayo si mazuri na yenye umbo baya wakati wa utengenezaji wa matunda pia upunguaji wa ukubwa wa tunda.

Angalizo; usimwagilie matikiti wakati wa jioni sana au usiku kwasababu inaweza kusababisha magonjwa ya majani kutokana na unyevu kukaa muda mrefu. Vile vile usimwagilie juu ya maua wakati wa asubuhi au join kwasababu unaweza kuzuia wadudu kama nyuki ambao ni muhimu sana wakati wa uchavushaji.

MAUA NA MATUNDA
Matikiti hutoa maua dume na jike kwenye tawi moja. Kwa kawaida maua dume huwa ni madogo zadi na hutoka mapema zaidi yakifuatiwa na maua jike ambayo huwa makubwa zaidi. Maua yanaweza yasionekane au yasitokee iwapo kiasi kidogo cha maji kitamwagiliwa ,upungufu wa viritubisho kwenye udongo na hali ya hewa ya joto/baridi sana n.k

Uchavushaji hufanya na wadudu na iwapo itaonekana hakuna wadudu unaweza kuchavusha kwa kutumia mkono.
Hii hufanywa kwa , kukata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji kwenye maua jike, maua jike ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora zaidi, unaweza kukata tawi lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii husababisha kuwa na matunda makubwa zaidi. Hii inawezwa kufanywa zaidi wakati wa Asubuhi.

MAGONJWA NA WADUDU
Wadudu wa matikiti wako wa aina mbalimbali na wanaoshambulia sehemu wanaoshambulia majani na maua, na wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea. Magonjwa kama Ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy mildew) na mengine yathibitiwe kabla hayajaleta madhara kwenye mimea.Ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi. Dawa aina ya Mancozeb inaweza kutumiwa kuthibiti ugonjwa magonjwa hayo hapo juu.
Vilevile matikiti hushambuliwa na wadudu ambao hukaa katika majani, maua na matunda.
Dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda.

UVUNAJI MATIKITI
Kabla ya kuvuna matunda ni vema kwanza kujua kuwa matikiti huchukua takribani miezi mitatu mpaka mitano toka inapopandwa mpaka kukomaa. Hii hutegemea na aina ya matikiti yenyewe. Tikiti lililo komaa linaatakiwa na mwonekano wake huwa kama ifuatavyo;

Rangi ya mng’ao hupotea
Upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi ya njano
Pia kikonyo juu ya tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu.
Ila njia nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na kusikiliza mlio wake unakuwa kama mlio wa ngoma.
Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti, yabebwe na kuhifadhiwa vizuri kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi binafsi

Soko la matikiti maji
Ukubwa wa tikiti na mwonekano wake ni baadhi ya sifa zinazoangaliwa na wananuzi. Matikiti madogo sana huwa hayapendi sana na wanunuzi. Kwa Tanzania wakulima wengi wanauza matikiti katika masoko ya ndani yanayopatikana takribani nchi nzima. Kwa miaka kadhaa tikiti moja limekuwa likiuzwa kwa wasitani wa shilling 1000 kwa tikiti dogo mpaka 3000 kwa tikiti kubwa katika masoko.

Mavuno
Mavuno ya matikiti yanategeme huduma za shamba pamoja na hali ya hewa. Matikiti pia hutofautiana katika mavuno kulingana na aina ya matikiti. Kwa wastani matikiti yanaweza kutoa kutoa mavuno kati ya TANI 15-36 kwa hekta moja.

July 30, 2018

Jinsi ya kutengeneza sabuni ya mche

Malighafi 

1. Caustic soda vijiko 27 vya chakula 

2. Maji chupa 239 soda 

3. Mafuta lita 2 ( mafuta ya nazi,mawese,nyonyo au mbosa) 

4. Sodium cilcate 1/

2 kg 

5. Rangi ya sabuni kijiko 1 cha chai 

6. Industrial salt vijiko 3 vya chakula 

7. Harufu kijiko 1 cha chai 

8. Hydrogen peroxide vijiko 4 vya chakula (kwa ajiri ya kuondoa rangi ya mafutu. 

Hatua 

1. loweka caustic kwenye maji kisha korog a kwa dk 5 na uache kwa kati ya siku 1 hadi 7 

2. siku ya kutengeneza sabuni injika mafuta jikoni na yakichemka tia hydrogen kidogokidogo huku 

ukiyaangalia mafuta yako kwa kutumia karatasi nyeupe kama rangi imetoka yote. 

3. Baada ya hapo chukua maji ya caustiki soda,tia sodium,chumvi,kama unapenda rangi weka na 

kama unapenda harufu weka huku nukikoroga kwa nguvu na kwa spidi hadi dk 5. 

4. Andaa ndoo ya plastiki na utie mafuta uliyoyaandaa na hakikisha yamepoa.anza kuyakoroga 

kuelekea upande mmoja huku ukimimina ule mchanganyiko wako wa causiki kwenye mafuta kwa 

mchuruziko kidogokidogo huku ukikoroga kwa nguvu zako zote hadi utapomaliza na baada ya dk 

10 hadi 15 hivi mkorogowako utakuwa tayari. 

5. Kamimine kwenye umbo na usubili sabuniikauke na baada itakuwa tayari kwa matumizi.

Vipimo vya ujenzi wa Banda la kuku 300 na stoo ya chakula

Kutuhusu ebusol

ebusol..Ni taasisi binafsi iliyosajiriwa kisheria kwa lengo la kuifikia jamii isiyofikiwa mjini na 

vijijini kuhamasisha, kuwaunganisha na kuwajengea uwezo kwa kutoa elimu na mafunzo ya 

UJASIRIAMALI NA STADI BORA ZA BIASHARA.

Mafunzo haya yanalenga kutoa ujuzi na taaluma katika maeneo yafuatayo:

1. STADI ZA MWEZESHAJI NA UWEZESHAJI

2. STADI ZA MPANGO WA MAISHA KWA VIJANA WENYE MALENGO

3. UONGOZI NA UTAWALA BORA

4. UJASIRIAMALI NA STADI BORA ZA BIASHARA

5. HATUA ZA USAJIRI WA BIASHARA

6. FURSA MBALIMBALI ZA BIASHARA TANZANIA

7. MAPISHI MBALIMBALI NA MAPAMBO KIBIASHARA

8. UFUGAJI BORA NA RAHISI KISASA KIBIASHARA

9. KILIMO BORA NA RAHISI CHA MBOGAMBOGA, MATUNDA NA MAZAO YA VIUNGO KIBIASHARA

10. UTAYARISHAJI,USINDIKAJI, UFUNGASHAJI NA UHIFADHI WA MBOGAMBOGA, MATUNDA NA MAZAO YA VIUNGO KIBIASHARA

11. UHAMASISHAJI, UUNDAJI NA UBORESHAJI WA VIKUNDI VYA MAENDELEO NA VICOBA

Kutuhusu ebusol

Hivi ndivyo chilly sauce inavyotengenezwa

CHILLY SOUCE

Malighafi

1. Pili pili mbuzi nyekundu kilo 1

2. Nyanya kilo 4

3. Vitunguu saum vikubwa 4

4. Mafuta ya kupikia vijiko 12 vya chakula 

5. Maji ya moto kikombe 1

6. Cetric acid kijiko 1 cha chakula

7. Vinegar vijiko 5 vya chakula.

Hatua

1. Menya nyanya na utoe mbegu za ndani ubaki na nyamanyama tu kisha changanya 

malighafi zote na usage kwenye blenda mpaka iwe rojorojo kabisa

2. Injika mafuta vijiko 30 vya chakula na yakianza kuchemka mimina mchanganyiko wako 

humo huku ukikoroga kuelekea upande mmoja wa dk15 au zaidi naukiona imekuwa uji 

uji acha na uipue.pooza na uweke kwenye vifungashio vyako tayari kwa kuuza.

Pata wazo Bora la biashara

Watu wengi wamekuwa wakiangaika hama kuwauliza watu wao wa karibu ni biashara gani afanye au ukimuuliza ni biashara gani unataka kufanya atakuambia mimi nataka kufanya biashara yoyote ili mradi tu iwe inaniingizia faidi. Kuwa maalum(specific) na usipende kufanya biashara yoyote kwani kama ujui unataka kwenda wapi basi uelekeo wowote utakupeleka usipotaka. Si mawazo yote yatakuwa sawa kwako,chagua wazo moja tu la biashara  na uanze kulifanyia kazi na uanze sasa kwa kutumia chochote ulichonachoo usingoje kuwa na fedha nyingi ndiyo uanze.Chagua eneo gani upo vizuri na kuchukua hatua sasa.

1.Kununua Mashine za kukoroga zege na kukodisha.

2.Kununua Mashine za kukata vyuma na kuzikodisha.

3.Kutengeneza na kuuza tofali.

4.Ufundi, Website updating/Database: Katika Halmashauri, Manispaa, Mashule, Wizara, Wilaya na Makampuni mbalimbali.

5.Kuanzisha kituo cha redio na televisheni.

6.Kufunga na kutengeneza vifaa mbalimbali vya electroniki na mawasiliano mfano; compyuta na vifaa vya compyuta na mawasiliano.

7.Kuuza software; mfano Antivirus, Operating Systems, Pastel, Tally, Myob, n.k

8.Kushona na kuuza nguo.

9.Kufungua Duka la kuuza nguo mpya; suit, socks, batiki, nguo za asili, Mashuka, Mashati, Suruali.

10.Ufugaji wa mifugo mbalimbali mfano Kondoo, Mbuzi, Ng?ombe, Kuku, Bata, na wengine.

11.Kufungua stationery, kuuza (supply) vitabu na vifaa mbalimbali ktk mashule na vyuo.

12. Kutoa ushauri mbalimbali waKitaalamu.

13.Kuuza viazi, mahindi, mihogo, kutengeneza popcorn na kuziuza.

14.Kusajili namba za simu na kuuza vocha

15.Kuwa na mradi wa Pikipiki zisizotumia mafuta na zinazotumia mafuta

16. Kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na hali ya hewa ya sehemu husika.

17.Kuuza Mitumba.

18.Kusimamia miradi mbalimbali

19.Kufungua duka la kuuza mitambo mbalimbali.

20.Kufungua banda la chakula na chips.

21.Kukodisha turubai viti na meza.

22.Kufungua Supermarket.

23.Kufungua Saluni.

24.Kufungua Bucha.

25.Video Shooting & Editing.

26. Kufungua Internet cafe.

27.Duka la kuuza matunda.

28.Kufungua duka la kuuza vifaa vya simu za mkononi na landline.

29.Kufungua duka la vifaa vya ujenzi; cement, vifaa vya umeme, duka la mabati.

30.Kutengeneza michoro mbalimbali ya majumba na miradi ya ICT.

31.Kuchapa vitabu, bronchures, n.k32.Kuanzisha kampuni ya ujenzi (Building contractor).

33.Kuuza Vifaa vya umeme wa nishati ya jua (solar) ,battery, inverter na vifaa vingine vya solar n.k.

34.Kuuza maji kwa jumla na rejaleja.

35.Kutengeneza na kuuza Unga wa lishe bora.

36.Kukodisha Music

37.Kuanzisha Mradi wa Taxi

38. Kuanzisha mradi wa Daladala.

39.Kuuza vifaa vya Kompyuta, laptops, converters, HDDs, Monitors, Softwares, CD Copiers na vifaa vingine.

40. Kununua magenerator na kukodisha

41.Kufungua kampuni ya kutoa huduma za simu.

42. Kufungua kampuni ya kutoa huduma za internet (ISP).

43.Kuuza mabati na vigae

44.Kujenga apartments

45. Kufungua Kisima cha mafuta ya taa au mafuta ya aina zote.

46.Kufungua Duka la samaki.

47.Kufungua Duka la nafaka.

48.Kufungua Shule za Awali, Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo.

49.Kujenga hostel

50.Kuuza vocha na vingamuzi vya DStv, Zuku, Startimes, Easy TV, TNG, Digitech, Continental.

51.Kujenga mtambo wa kuzalisha umeme na kuuza katika viwanda na wananchi.

52.Ufundi simu

53.Kufungua Hospitali, Zahanati.

54.Maabara ya Macho, Meno

55. Kuchimba/Kuuza Madini

56.Kufungua ofisi ya kutoa huduma ya simu na fax.

57.Kuuza miti na mbao.

58.Kufungua Grocery, bar

59.Kufungua studio ya kupiga na kusafisha picha.

60.Kucharge simu/battery.

61.Duka la TV na vifaa vingine.

62.Kuanzisha biashara ya kuuza vyakula katika sherehe na tamasha mbalimbali (catering).

63.Banda la kupigisha simu.

64.Kuuza na kushona Uniform za shule.

65.Kuanzisha duka la kuuza vitu kwa jumla.

66.Kufungua gereji za kutengeneza bajaji, pikipiki na magari

67.Kuuza vyuma, pembejeo, rake, jembe

68.Kuuza fanicha.

69.Kufungua sehemu ya kuziba pancha za matairi ya magari na mitambo.

70.Kujenga nyumba za kulala wageni (hotel)

71.Kuagiza na kuuza vifaa vya aluminium.

72.Kuuza vioo

73.Kushona na kukodisha nguo za harusi.

74.Kufungua yard kwa ajili ya kuosha magari

75.Kuuza mashine za kuchomelea (welding machine).

76.Kuuza vifaa vya kuvaa Site (boots, helmets etc)

77.Kununua mabasi kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi

78.Kufungua studio ya kutengenezavipindi vya redio na televisheni

79.Kuanzisha ofisi ya michezo ya televisheni (TV Games)

80.Kufungua benki.

81.Kuwa na malori ya kubeba kokoto na mchanga.

82.Kuuza vifaa mfano TV, CCTV Camera, n.k

83.Kuwa dalali wa vitu mbalimbali.

84.Kuanzisha mradi wa kukodisha fork lift na winchi (crane)

85.Kuanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu.

86.Kuanzisha viwanda mbalimbali

87.Duka la vifaa vya simu na gadgets mbalimbali zinazoendana na mawasiliano ya Vodacom, TTCL, AIRTEL, TIGO, ZANTEL, n.k.

88.Kujenga Ukumbi wa kukodisha kwa sherehe, mikutano mbalimbali

89.Kununua matrekta, mitambo ya ujenzi wa barabara na kukodisha

90.Kutengeneza antenna na kuuza

91.Kufungua mradi wa Machine za kusafisha, kutoboa na kuchana mbao

92.Kufungua mradi wa kuuza vifaa vya Umeme wa kutumia upepo

93.Biashara ya kuagiza magari

94.Kufanya biashara za Jukebox

95.Kukodisha matenki ya maji

96.Kufungua duka la kuuza Asali

97.Kutengeneza Mikokoteni/ matoroli na kuikodisha

98.Kufungua Duka la vinyago, batiki

99.Kuanzisha huduma ya AIRTEL MONEY, MPESA, TIGOPESA, EZYPESA

100.Kuanzisha sehemu ya kufanyia mazoezi (Gym).

101.Kununua na kuuza vifaa vya kupima ardhi.

102.Kufungua duka la kuuza dawa (pharmacy).

103.Kufungua Kampuni ya Ulinzi

104.Kufungua kampuni ya”Clearing and fowarding”

105.Kuchezesha vikaragosi

106.Kuuza spea za bajaji, magari na pikipiki

107.Kuuza baiskeli

108.Kuuza magodoro

109.Kuuza vyombo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya nyumbani mfano bakuli, sahani, vikombe,vijiko,

110.Kuuza marumaru (limestones)

111.Kuuza kokoto

112.Kuuza mchanga

113.Kufundisha Tuisheni

114.Biashara za bima

115.Kampuni ya kusafirisha abiria kwa njia ya anga (ndege)

116.Biashara za kitalii

117.Biashara za meli na maboti.

118.Kampuni ya kuchimba visima

119.Kufungua ofisi ya wakili/mawakili wa kujitegemea

120.Kuuza mkaa

121.Kutengeneza mashine za kutengeneza tofali

122.Kampuni ya kupima ardhi

123.Kampuni ya magazeti

124.Kuchapa (printing) magazeti

125.Kuuza magazeti

126.Kuchimba mafuta

127.Kiwanda cha kutengeneza mabati

128.Kiwanda cha kutengeneza fanicha

129.Kiwanda cha kutengeneza matairi

130.Kutengeneza vitanda vya chuma

131.Kununua nyumba katika Maghorofa (Apartments) na kuzikodisha.

132.Kukodisha makapeti

133.Kupamba maharusi na kumbi za harusi/sherehe.

134.Mashine ya kusaga na kukoboa nafaka.

135.Kazi ya ususi na kusafisha kucha.

136.Kuuza Gypsum

137.Malori ya kubeba mafuta na Mizigo

138.Duka la kuuza mboga za majani

39.Duka la kuuza maua.

140.Kampuni ya kuzoa takataka

141.Kampuni ya kuuza magari

142.Kuuza viwanja

143.Uvuvi

144.Kutengeneza na kuuza nguzo za kujengea fensi

145.Uchoraji wa mabango.

146.Duka la kuuza silaha

147.Ukumbi wa kuonesha mpira

148.Biashara ya Multi-Level Marketing-MLM

149.Yadi kwa ajili ya kupaki magari

150.Mradi wa trekta za kukodisha kwa ajili ya kilimo..

Amua haraka nini unataka kufanya nini kwa ajili yako na maisha yako na kama kweli unataka kufanya biashara/ujasiriamali  napenda kukusisitiza uanze sasa kwa kutumia chochote ulichonacho kwani ndege mmoja aliyo mkonono mwako ni bora zaidi kuliko 100 walio angani

By Ombeni haule

July 29, 2018

Kilimo Cha muhogo Ni fursa



Je wajua China na Tanzania zimesaini Mkataba wa Soko la Mihogo? Kama hufamu basi nikuelezee kwa ufupi. Ni hivi, Nchi ya China ni moja ya nchi zinazotumia sana zao la muhogo. China imeingia mkataba na Serikali ya Tanzania wa soko la mihogo, ambapo Tanzania itapaswa kuuza China mhogo Tani laki moja (100,000) kwa mwaka. Hata hivyo toka mkataba huo usainiwe hadi leo mwaka mmoja tayari umepita. Ila kwa mwaka wa kwanza, Tanzania tulifanikiwa kuuza tani 10,000 pekee (sawa na asilimi 10% tu ya kiasi kinachohitajika). Hivi karibuni nilimsikia Balazi wa China nchini Tanzania, Wang Ke akisema, licha ya kuingia makubaliano na Tanzania ya kununua tani 100,000 za mihogo kwa mwaka, kwa sasa wanapata tani 10,000 pekee. Pia akashauri kuwepo kwa ushirikiano baina ya serikali, sekta binafsi na wakulima ili mihogo mingi izalishwe.

Hapa chini nimekuwekea somo kuhusu Kanuni Za Kilimo Bora Cha Muhogo

Utangulizi

Muhogo ni zao linaoongoza kwa kulimwa sana kwa nchi za ukanda wa jangwa la Sahara. Katika nchi hizi, zao la muhogo limeendelea kuwa zao la kitamaduni kwakuwa limekosa msaada wa kutambulika au kuwekewa mkazo zaidi na viongozi wa nchi hizi kutokana na sifa zake nyingi ambazo mazao mengine hayana. Zao la muhogo ni moja kati ya mazao ambayo hutumika kama zao la biashara na wakati huohuo ni zao la chakula. Wakulima wengi wamekuwa na uelewa finyu wa mbinu bora za kilimo katika kuzalisha mazao mengi ya muhogo. Kwa Afrika muhogo hulimwa sana Nigeria, Congo DRC, Zambia, Ghanana Tanzania. Kwa hapa Tanzania, muhogo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuna, Tanga, Morogoro, Shinyanga na mikoa mingine kwa uchache. Zao hili lina kiwango kikubwa cha wanga ukilinganisha na nafaka (asilimia 40 zaidi ya mchele, asilimia 25 zaidi ya mahindi). Majani yake hutumika kama mboga na yana virutubishi muhimu hususan vitamini B na protini. Kwa hapa nchini uzalishaji wake ni wastani wa tani milioni saba kwa mwaka kwa takwimu zilizopo. Wazalishaji wengi kwa hapa nchini ni wakulima wadogo wadogo au vikundi vya wakulima ambao hawana elimu au uelewa au utaalamu mkubwa katika uzalishaji wa zao hili. Hali hii ndiyo inayopelekea zao la muhogo au hata mazao mengi kutoka nchi za Afrika kukosa ushindani katika masoko ya kimataifa kwakukosa ubora au kuzalishwa kwa uchache tena na wakulima wadogo wadogo wachache.

Kijarida hiki kinalenga kutoa mwongozo kwa wakulima wadogo na wakubwa, vikundi vya wakulima, maafisa ugani na hata wawekezaji wanaotaka kujikita katika kuzalisha muhogo au mbegu za mihogo kwa matumizi mbalimbali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali. Kitabu hiki kitamwezesha msomaji kujua hatua kwa hatua juu ya mbinu bora na za kisasa za uzalishaji wa muhogo. Ni mategemeo ya waandishi kuwa kijarida hiki kinatoa mchango mkubwa katika kubadilisha mtazamo wa wakulima na kuwasaidia kuacha kulima kwa mazoea na kuanza kulima kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha muhogo zilizofanyiwa utafiti na ambazo tayari zimewafikia wadau.

 

Mambo Yamsingi Ya Kuzingatia Katika Uzalishaji Wa Muhogo.

Ili kupata mazao mengi na bora ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha mihogo kama ifuatavyo:-

 

  1. Aina ya Udongo na Mazingira ya Muhogo.

Zao la Muhogo ni moja kati ya mazao ya chakula na biashara ambalo hustahimili ukame na huweza kuhimili hata katika udongo usio na rutuba ya kutosha ambapo mazao mengine kama Mahindi yasingeweza kustawi. Joto linalofaa Zaidi kwa ustawi wa muhogo ni kati ya nyuzijoto 25-30. Muhogo hudumaa ikiwa joto litapungua kufikia nyuzi 10 au chini kwani haiwezi kustamihili baridi kali, hasa ukungu kwa muda mrefu katika kipindi chake cha ukuaji.Kiwango cha mvua kwa mwaka kinachokubalika kwa muhogo ni kati ya milimita 1000-1500 na hasa wakati wa miezi 3 ya mwanzo. Pia muhogo unahitaji udongo mwepesi wenye asili ya kichanga na tifutifu usiotuamisha maji na unastawi zaidi katika mwinuko wa 0-1000m kutoka usawa wa bahari.

 

  1. Uandaaji wa shamba

Shamba huandaliwa kwa kufyeka, kung’oa visiki na ikibidi kuchoma moto na kukatua (kutifua) kutegemeana na hali ilivyokuwa. Baada ya shamba kuwa safi upandaji hufuatia.Muhogo unaweza kupandwa kwenye sesa au matuta.Sesa inafaa katika sehemu tambarare ilihali matuta yanatumika katika ardhi ya tambarare au mteremko.

 

  1. Uchaguzi wa mbegu na upandaji wa muhogo

Uchaguzi wa mbegu Kwa kawaida, muhogo hupandwa kwa kutumia vipande vya miti ya muhogo vyenye urefu wa sm 20 – 35. Mbegu ya muhogoinapaswa isiwe na vikovyo pungufu ya vitatu licha ya urefu wake kwani hiyo ndiyo sehemu ambayo mizizi na shina huchipua. Chagua mbegu kutoka kwenye shina lililokomaa vyema na lisilo na dalili ya magonjwa. Pia katika kuandaa mbegu, sehemu ya juu na chini ya ufito wa muhogo haifai kupandwa. Wakati wa kuchagua mbegu, zingatia yafuatayo:

  • Chagua mbegu bora yenye ustahimilivu/ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu
  • Chagua mbegu inayozaa sana
  • Chagua mbegu inayohitajika sokoni
  • Chagua mbegu inayoweza kustahimili muda mrefu bila kuharibika kabla ya kuvunwa
  • Wakati wa kuandaa mbegu, hakikisha vikonyo (nodes) na ngozi ya mche havichuniki/haviharibiki
  1. Upandaji wa muhogo

Njia kuu za kupanda muhogo ni wima (vertical), kuinamisha (slanting) au kulaza (ulalo) na kuifukia yote (horizontal). kiwango cha kuzamisha mbegu hiyo ni robo tatu ya kipande husika kwa njia za wima na mwinamo. Endapo njia ya ulalo itatumika, mbegu ilazwe na kufukiwa yote kwa kiwango cha sentimita 10, japo sentimita 5 – 20 pia zinaweza kutumika. Sentimita 2.5 hadi 4 ni unene unaofaa kwa mbegu za muhogo. Panda kwenye matuta au kwenye sesa kulingana na matakwa ya shamba lako. Nafasi kati ya mstari mmoja hadi mwingine ni mita 1. Umbali huo pia hutumika kati ya shina na shina. Hata hivyo umbali huu unaweza kubadilika hadi kufikia mita 1.5 kati ya mstari na mstari na mita 1 kati ya shina na shina ikiwa muhogo utachanganywa na mazao mengine kama vile karanga , mahindi, njugu au kunde. Ikiwa ni kwaajili ya uzalishaji wa mbegu mara nyingi vipimo hupungua zaidi na hata kufikia mita 0.5 kwa 0.5. Mbegu ya muhogo ni vema ikafukiliwa vizuri kama mkulima hatumii mashine ya kupandia.

*Uongezekaji wa mazao ya muhgo kuanzia 20-45t/ha huanzia kwenye hatua hii ngumu ya utunzaji na uangalizi wa mbegu, hivyo basi Mkulima hana budi kufuata hatua hizo zilizolizopendekezwa ili aongeze mazao*

  1. Upandaji wa Mihogo kwa kutumia mashine/Mitambo ya Kupandia

Kupanda mihogo kwa kutumia mashine au mitambo maalumu ya kupandia mara nyingi hutumika katika mashamba makubwa (large scale farming). Kwa Tanzania teknolojia hii haijawafikia wakulima walio wengi japokuwa kuna taasisi kama IITA zikishirikiana na Chuo Kikuu Cha Kilimo (SUA) ambazo zimeanza kufanyia utafiti na majaribio hapa nchini. Mitambo hii mara nyingi hufungwa na hukokotwa na trekta lenye nguvu kati ya 70-90 horsepower (hp).
Kutegemeana na aina ya mashine ya kupandia mihogo, mbegu za mihogo hukatwa kati ya sentimita 20 hadi 25. Mbegu zinatakiwa kuwa katika urefu na unene ulio sawa. Wataalamu pia wameshatengeneza mashine maalumu za kukatia mbegu za mihogo.Watu wawili au wanne (kutokana na aina ya mashine) huweza kukaa nyuma kabisa ili kufanya zoezi zima la upandaji, ikiwa ni dereva wa trekta, wapakiaji mbegu na watiaji mbegu katika mashine

Baadhi ya mashine za kupandia mihogo hufanya kazi zote kwa wakati mmoja yaani hukata mbegu katika vipimo sawa, hupanda kwa vipimo sawa, huweka mbolea, na kufukia mbegu ya muhogo. Mara nyingi aina hii ya mashine huweza kupanda hekta 3 hadi 6 kwa siku wakati zile ambazo hulishwa mbegu zilizokwisha kukatwa huweza kupanda hekta 7 hadi 10 kwa siku.

*Mashine zilizotengenezwa kwa kazi hii hupunguza gharama za vibarua. Utumiaji wa mashine ni mzuri na hupunguza gharama za upandaji kwa zaidi ya 50% dhidi ya upandaji kwa mkono. Gharama kubwa za uendeshaji wa mashine hizi bado siyo rafiki kwa mkulima mdogo. Nchi kama Nigeria, Ghana na nyinginezo wana taasisi ambazo hukodisha mashine hizi kwa wakulima kwa gharama nafuu*

  1. Upandaji wa muhogo na mazao mengine (Intercropping)

Hakuna ubaya au madhara yoyote kwa kuchanganya muhogo na mazao mengine kama vile karanga, maharage, mahindi na mengineyo jamii ya mikundekunde (legumes). Upandaji wa mchanganyiko ni matumizi mazuri ya ardhi, huzuia mmomonyoko wa ardhi, huongeza rutuba ya asili, n.k.Mara nyingi Mkulima anashauriwa kuandaa matuta ikiwa atapenda kupanda muhogo na mazao mengine. Muhogo upandwe juu ya tuta na mazao mengine yapandwe pembeni ya tuta na umbali wa kupanda mbezu za muhogo uwe mita 1×1 ili kuruhusu mazao mengine yakue pia vizuri. Hata hivyo, ulimaji huu huweza pia kufanywa katika sesa ambapo nafasi kati ya mstari na mstari usipungue mita moja na nusu.

  1. Upandaji wa mbegu kwa Wakati Muafaka

Wakulima wanashariwa kupanda mbegu za muhogo kwa wakati sahihi ili kujihakikishia mavuno mazuri. Mkulima hashauriwi kupanda muhogo wakati wakiangazi/ukame au wakati mvua zinaishaisha au pale ambapo kina cha maji katika ardhi kipo chini sana. Hii ni kwa sababu mbegu zinahitaji unyevunyevu kidogo wakati wa kupandwa ili kuruhusu miche ichipuke na kupunguza mashambulizi dhidi ya mchwa. Kiuhalisia, muhogo unatakiwa kupandwa katika kipindi kitakachoruhusu upatikanaji wa unyevunyevu kwa kipindi cha angalau miezi miwili au mitatu mfululizo.

  1. Matumizi ya Mbolea au virutubisho katika upandaji wa Mbegu za Muhogo

Kwa muda mrefu, dhana ya matumizi ya mbolea katika kilimo cha muhogoilikuwa haijazoeleka miongoni mwa wakulima wengi. Hii ilitokana na kutokuwepo na tafiti mahsusi juu ya aina na viwango vya mbolea inayotakiwa kutumiwa katika uzalishaji wa muhogo. Mradi wa taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha nchi za ukanda wa joto (IITA) chini ya mradi wake wa SARD-SC ikishirikiana na taasisi za utafiti wa Kilimo chini ya Wizara ya Kilimo Tanzania, zimekuwa zikifanya utafiti juu ya matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa muhogo. Matokeo ya awali yanaonesha mafanikio katika kuongeza uzalishaji wa muhogopindi mbolea sahihi inapotumika kwa viwango sahihi. Hata hivyo, wakati matokeo rasmi ya tafiti hizi yakiendelea kusubiriwa, inashauriwa wakulima waendelee kulima kilimo cha mpishano na mchanganyiko wa mazao ya jamii mikunde ili kuongeza rutuba ya asili. Kwa wakulima wakubwa ambao wanahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa ni vema wakawaona maafisa kilimo kwa ushauri ili kuweza kutumia mbolea hizi kwa usahihi ili kuongeza tija.

  1. Udhibiti wa Magugu katika Muhogo

Magugu huweza kupunguza uwezo wa mizizi (muhogo) kukua na kuzaa kwa asilimia kati ya 40 hadi 70. Baadhi ya magugu huweza kupenya katika muhogona kuacha upenyo unaoweza kuruhusu wadudu wanaosababisha magonjwa kuingia kwa urahisi, hivyo udhibiti wa magugu ni muhimu katika kupunguza uwezekano wa muhogo kushambuliwa na magonjwa. Katika shamba la muhogo, kazi ya kupalilia huchukua zaidi ya asilimia 60% ya kazi zote kuanzia kupanda hadi kuvunana pia huchukua zaidi ya asilimia 40% ya gharama zote za uzalishaji. Ili kudhibiti magugu, muhogounatakiwa kupaliliwa angalau mara 2 au 3 na zaidi kutegemeana na hali ya shamba na ukuaji wa magugu. Hapa tutaangalia njia bora, sahihi na zenye gharama nafuu katika kukabiliana na magugu katika mashamba ya muhogo. Magugu yanayoshambulia mashamba ya muhogo yamegawanyika sehemu kuu mbili, magugu ya msimu na magugu ya muda mrefu.

  1. Muda sahihi wa kupalilia shamba

Shamba linapaliliwa magugu ili kuruhusu muhogo ukuwe vizuri na kupunguza ushindani wa virutubishi kati ya mazao na magugu. Palizi ifanyike mara kwa mara mpaka mihogo inapokomaa. Mkulima anashauriwa kuhakikisha shamba lake halina magugu kwa kupalilia mara kwa mara hasa miezi 4 ya kwanza baada ya kupanda. Endapo shamba litakuwa jipya au lipo bondeni au kwenye mazingira yenye visababishi vingi vya magugu kuota mkulima anashauriwa kupalilia shamba lake mara kwa mara kila magugu yanapoota. Kwa wakulima wakubwa mara nyingi muhogouliopandwa kwa mashine hupaliliwa kwa mitambo maalumu ya kupalilia.

  1. Namna ya kukabiliana na Magugu

Kuna njia kuu tatu za kukabiliana na magugu: Biolojia, kitamaduni/mazoea na kemikali.

  1. Kibiolojia: Kukabiliana na magugu kibiolojia maana yake ni kuyafanya magugu yasiote shambani kwa kupanda mimea mingine
  2. Kitamaduni/Mazoea: Njia bora za kilimo inapunguza idadi au madhara ya magugu katika mimea. Njia zilizozoeleka ni kutumia jembe la mkono, kuchoma, kufunika shamba, kuweka mbolea.
  3. Kemikali: Madawa ya kudhibiti magugu huua au kuharibu kabisa magugu. Dawa hizi huweza kuwekwa kabla ya kulima shamba au mara baada ya kuandaa shamba au miezi michache baada ya kupanda. Matumizi ya kemikali husaidia kuzuia au kuua magugu magumu ambayo ni vigumu kung’oa kwa mikono au jembe la mkono, pia huzuia kuharibika kwa muhogo ulio ardhini,na kuzuia magugu yanayokua kwa kasi. Kemikali hizi pia huweza kutumika kabla ya kupanda, wakati wa tahadhari na baada ya kupanda. Kwa Tanzania bado tafiti zinaendelea kuhusiana na matumizi sahihi ya hizi dawa katika kuangamiza magugu, na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa utumiaji wa kemikali katika kuangamiza magugu hupunguza gharama za palizi kwa zaidi ya 50%. Kwa nchi zilizoendelea mara nyingi huzalisha muhogo, kwaajili ya matumizi ya viwandani hivyo hutumia kemikali katika kuangamiza magugu. Kwa nchi nyingi za Afrika muhogo mwingi hutumika kwaajili ya chakula na kiasi kidogo sana ndio hutumika viwandani.

*Wakulima wakubwa wanashauriwa kuwaona maafisa kilimo wa sehemu husika au IITA na taasisi nyingine kwa maelezo na utaalamu juu ya matumizi ya kemikali katika kuangamiza magugu maana elimu na utaalamu vinahitajika katima matumizi sahihi ya hizi kemikali*

  1. Udhibiti wa magonjwa na wadudu

Kilimo cha muhogo Tanzania kinakabiliwa na changamoto ya magonjwa ya aina mbalimbali kama ilivyo kwa mazao mengine. Muhogohushambuliwa sana na magonjwa na wadudu.Wadudu hao ni kama utitiri wa kijani wa muhogo, vidung’ata, vidugamba weupe, na mchwa. Kwa upande wa magonjwa, muhogohushambuliwa zaidi na batobato, mizizi kuoza na Michirizi ya kahawia. Kwa pamoja magonjwa na wadudu huweza kusababisha hasara ya upotevu wa mazao kwa zaidi ya 50% kwenye muhogo. Sababu kuu ya kuendelea kuwepo kwa haya magonjwa ni matumizi ya mara kwa mara ya mbegu zisizo na ubora zinazoweza kukinzana na magonjwa na wadudu waharibifukama vile ugonjwa wa batobato (CMD)ambao huambukizwa Batobato Michirizi ya kahawia zaidi ya 81% kwa njia ya mbegu
zilizo na vimelea vya ugonjwa huu. Dalili za Ugonjwa huu ni; Mabaka mabaka kwenye majani, majani kujikunja na kupoteza umbo lake, majani kuwa magumu kuliko kawaida, mmea kudumaa, na mmea kunyauka na hatimaye kufa. Ugonjwa wa Michirizi ya Kahawia (CBSD) kwa Tanzania huonekana zaidi katika ukanda wa bahari ya Hindi kama vile Mtwara, Pwani, Lindi japokuwa hivi karibuni ugonjwa huu pia umeonekana pia katika Kanda ya Ziwa kama vile Kigoma, Ukerewe na pembezoni mwa ziwa Victoria. Dalili za ugonjwa wa michiriz ya kahawia kwenye majani ya mmea wa muhogo ni; michirizi ya kahawia au mabaka ya kahawia kwenye mistari ya vena, mmea kudumaa na kunyauka.Kwa upande mwingine, dalili za ugonjwa huu katika mizizi au muhogo wenyewe ni; Rangi ya kahawia muhogo unapokuwa umekatwa na muhogo kupoteza umbo lake. Kutokana na kuwepo kwa magonjwa makuu yaliyotajwa hapo juu, yafuatayo ni muhimu yakazingatiwa ili kudhibiti magonjwa katika muhogo:

  • Kutumia mbegu bora zenye ukinzani na magonjwa tajwa kama zilivyofanyiwa utafiti na taasisi mbalimbali za utafiti wa kiliomo.
  • Kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora zenye ukinzani kwa kuanzisha mashamba ya uzalishaji mbegu katika maeneo mbalimbali.
  • Kuacha kutumia mbegu za zamani ambazo kwa kiasi kikubwa tayari zimeathiriwa na magonjwa haya.
  • Kuyatunza vema mashamba yao ya muhogo (proper farm management). Wakulima wengi hudhani muhogo ukishapandwa basi hauhitaji matunzo hivyo hutelekeza mashamba na hutegemea mavuno makubwa.
  • Kuchagua mbegu zisizo na maambukizi ya magonjwa.
  • Kung’oa na kuteketeza mimea yote iliyoathiriwa na magonjwa ikiwa bado shambani.
  • Kuteketeza kwa moto au kwa kufukia mimea yote iliyoathirika mara baada ya kuvuna.
  • Kutenga shamba la muhogoumbali wa angalau mita 50 kutoka mashamba mengine ya muhogoambayo yameathirika.
  • Kupanda muhogo kwa wakati.
  • Kutunza shamba la mihogo kwa kupalilia mara kwa mara hasa miezi minne ya kwanza mara baada ya kupanda.
  • Uvunaji mapema wa muhogounaweza kupunguza hasara itokanayo na magonjwa.

*Kuna magonjwa mengine ambayo pia hushambulia zao la muhogomashambani kama vile; majani kuwa na alama ya kikahawia (Brown leaf spot), Majani kuwa na alama nyeupe nyeupe (White leaf spot) n.k. lakini hayana madhara sana kiuchumi. Jambo la msingi ni kwa wakulima kukagua mashamba mara kwa mara ili kuona kama kuna mashambulizi na kuchukua tahadhari mapema kwa kung’oa mmea na kuutupa au kuufikia kabisa, maana dawa za magonjwa haya hakuna*

Mwisho

Zao la muhogo linajulikana kuwa ni moja ya mazao rahisi sana kuyalima japokuwa wakulima wengi hawana uelewa juu ya mbinu bora na sahihi za utunzaji wa shamba la muhogo. Mara nyingi muhogo umekuwa ukipandwa kwenye ardhi isiyofaa, isiyo na rutuba lakini bado mkulima huweza kuvuna japo si kwa kiwango kikubwa. Imefika wakati wakulima na wadau wengine walithamini zao la muhogo kwa kupanda kwenye udongo mzuri na wenye rutuba ili kuongeza mavuno. Kwa upande mwingine, mavuno mazuri ya muhogohutegemea mbegu nzuri na zenye ukinzani na magonjwa, zilizopandwa kwa wakati, shamba lililotunzwa vizuri kwa kupalilia kila wakati magugu yanapotekea na kukagua shamba mara kwa mara. Kwakuwa kwa sehemu kubwa kilimo cha muhogo kinategemea mvua, kuchelewa kupanda kunaweza kusababisha muhogo kutoota au kutokukuwa vizuri. Muhogo uliopandwa kwa wakati na kutunzwa vizuri hutoa mazao mengi na bora na huo ndio ukulima bora wa muhogo. Ili kupata matokeo mazuri katika ulimaji wa zao la muhogo, ni muhimu kwa wakulima kufuata kanuni za kilimo bora cha muhogo kuanzia uandaaji wa shamba hadi kukua kwa muhogo. Kanuni bora za kilimo huanza kwenye kuchagua mbegu safi, zenye ukinzani na magonjwa, zinazozaa sana na kwa kupata mbegu kutoka kwenye mmea wa muhogouliokomaa vizuri. Wakulima wadogo wadogo watafute ushauri na huduma mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa kilimo cha muhogo kama wanavyofanya wafugaji. Matumizi ya mashine na kemikali katika kupanda na kuangamiza magugu ni teknolojia mpya ambazo wakulima wengi wa muhogohawajaanza kuitumia kwa hapa nchini. Ni rai yetu kwa serikali,taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo kuwekeza kwenye mashine ili kupunguza mzigo wa kuhudumia mashamba ya muhogo na matumiziya kemikali katika kukuza na kuangamiza magugu. Kwa pamoja mkulima anaweza akaondokana kabisa na jembe la mkono ambalo halina tija kwa mahitaji ya zao la muhogo kwakuwa hata nchi za bara la Asia zimeanza kuja Tanzania kutafuta muhogo.

Kilimo cha Muhogo ni suluhisho la tatizo la njaa, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi hapa Tanzania! Muhogo ni pesa, Muhogo ni Chakula