January 03, 2019

UTUNZAJI WA KITALU CHA BUSTANI

Na Ombeni Haule cdf

Baada ya kuandaa kitalu hakikisha unakitunza vizuri ili kuweza kupata miche bora ya kupandikiza shambani. Matunzo ya kitalu hujumuisha mambo yafuatayo;

Kujengea kichanja/Kivuli (Shading)

Umwagiliaji

Kupiga dawa za wadudu na magonjwa

Kupunguzia miche na

Kuitayarishaji miche kabla ya kuipandikiza.

(a) Kujengea kichanja / Kivuli

Mbegu zitakapoota ondoa matandazo na tengeneza kichanja chenye kimo cha mita 1 kutoka ardhini kilichotandazwa nyasi au makuti kufunika kitalu. Kichanja hiki hutengenezwa ili kuipa kivuli miche ambayo bado ni michanga isije kuungua na mionzi ya jua na kushindwa kukua vizuri. Vilevile kichanja husaidia kupunguza kasi ya matone ya mvua kubwa ili miche isijeruhiwe.

(b) Umwagiliaji

Mwagilia maji kitaluni kila siku asubuhi na jioni hadi wakati wa kutayarisha miche. Ni vyema kuzingatia uwezo wa udongo kutunza maji ili kuepuka kuzidi kwa kiwango cha maji kunakoweza kupelekea kudumaa kwa miche kitaluni na kuchelewesha upandikizaji.

(c) Kupunguzia miche

Punguza miche kitaluni ili kuondoa msongamano wa miche na kubaki na miche itakayoweza kukua vizuri kwa nafasi. Hili ni muhimu hasa kwa miche yenye majani mapana kama vile miche ya nyanya na kabichi. Miche ya kabichi hupunguziwa siku nne hadi wiki moja tangu mbegu kuota wakati miche ya jamii ya nyanya hupunguziwa baada ya wiki moja tangu kuota kwa mbegu. Miche iliyopunguzwa katika tuta moja inaweza kuhamishiwa katika tuta lingine.

(d) Kupiga dawa za Wadudu na Magonjwa

Unaweza kuanza kunyunyizia dawa za ukungu na kuua wadudu wiki moja hadi mbili tangu miche kuota. Chagua dawa kulingana na wadudu waharibifu na magonjwa yanayo shambulia zao husika. Hakikisha unafuata maelekezo ya dawa husika.

(e) Kuitayarisha miche (Acclimatization)

Miche hutayarishwa ili isipate tabu kuzoea hali ngumu ya shambani na hivyo kupona haraka inapopandikizwa. Utayarishaji wa miche hufanywa kwa kupunguza matandazo ya nyasi katika kichanja polepole kuanzia wiki mbili kabla ya kupandikiza. Ondoa kivuli chote na punguza kiwango cha maji ya kumwagilia wiki moja kabla ya kupandikiza ili kuiwezesha miche kuzoea hali ya ukame.

Zingatia: Usichelewe kupandikiza miche kwa sababu miche mikubwa ni vigumu kuihamisha na mizizi yake ni mirefu hivyo inaweza kukatika kwa urahisi. Pandikiza miche ikiwa na mizizi iliyozungukwa na udongngo

No comments:

Post a Comment