SIFA ZA ENEO ZURI LA UFUGAJI WA SAMAKI
SIFA ZA ENEO ZURI LA KUFUGIA SAMAKI Katika sehemu hii ya tatu tunaangalia ufugaji wa samaki hatua kwa hatua na katika hatua ya kwanza tunaangalia sifa 9 za eneo zuri la kufugia samaki kama zilivyoainishwa na Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dr. Berno Mnembuka ambaye pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji
Sifa ya 1 ni kuwa eneo la kufugia samaki linatakiwa liwe na maji ya kutosha kwa mwaka mzima. Hii ina maana kuwa eneo husika la bwawa linatakiwa liwe na maji ya kutosha kwa maana ya ujazo, chanzo cha maji kiwe ni cha kuaminika na kiwe kinakubalika kisheria, pia chanzo hicho cha maji kiwe kinaurahisi wa kupeleka maji kwa maana unapoyahitaji uweze kuyaelekeza yaingie bwawani na usipoyahitaji yaweze kutoka.
Sifa ya 2 kwa mujibu wa mtaalamu huyu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka ni kuwa eneo la kufugia samaki linatakiwa liwe na udongo unaoweza kutuamisha maji. Udongo wowote wenye asili ya mfinyanzi unafaa kwa kufugia kutokana na kuwa na tabia ya kushikamana na pia udongo huu hupenyeza maji ardhini taratibu na hivyo kusababisha maji kutuama kwa muda mrefu.
Eneo la kufugia samaki linatakiwa liwe na mwinuko au mteremko wa wastani, lisiwe la tambarare. Mteremko ni vema usiwe mkali sana ila uwezeshe maji kutiririka kuingia na kutoka bwawani. Eneo la tambarare kabisa si zuri sana kwani litakupa shida wakati wa uchimbaji na litasababisha uchimbaji wa bwawa kuwa kama kisima hivyo haitakuwa rahisi kuondoa maji toka bwawani pindi utakapohitaji kufanya hivyo.
Sifa ya 4 ya eneo zuri la kufugia samaki ni kuwa eneo lisiwe na historia ya mafuriko, kwa kuwa mafuriko yakitokea samaki waliokuwa bwawani wataondoka na maji na bwawa litafunikwa na udongo. Ili kujua historia ya eneo husika unaweza hata kuwauliza watu walioishi eneo hilo kwa muda mrefu.
5Sifa nyingine ya eneo zuri la kufugia samaki ni ile ya kuwa na eneo linalofikika kwa urahisi. Ni vizuri eneo liwe karibu na nyumbani au makazi ya watu ili kukuwezesha kutoa huduma kwa urahisi, pia kudhibiti wezi na maadui wa samaki.
Eneo la kufugia samaki pia linatakiwa kuwa ni eneo lenye amani na utulivu na watu wenye kuelewana. Mfugaji anatakiwa kuwekeza bwawa lake katika eneo ambalo kunakuwa na maelewano baina yake na wakazi wengine kinyume cha hapo iwapo hakutakuwa na maelewano maadui zako wanaweza
kuwadhuru samaki unaowafuga.
Sifa ya 7 ni kuwa na soko la bidhaa, iwapo mfugaji ataamua kufuga kwenye eneo ambalo lina soko la samaki basi itakuwa ni rahisi kwake kupata wateja na pia itampunguzia gharama za kusafirisha samaki kutoka eneo analofugia hadi eneo lingine kwa ajili ya kutafuta wateja.
Sifa nyingine kwa mujibu wa Dr. Mnembuka ni kuwa na umiliki wa ardhi wa uhakika. Kwa sababu shughuli ya ufugaji wa samaki ni ya muda mrefu mfugaji anatakiwa kuhakikisha kuwa ardhi anayoitumia ni ya kwake au ana umiliki nayo kwa muda mrefu ili isije ikatokea kabla ya mavuno au wakati ufugaji ndiyo unakomaa linajitokeza tatizo la mgogoro wa ardhi na hivyo ikamlazimu mfugaji kuhamisha bwawa lake.
Sifa ya 9 na ya mwisho ni uwezekano wa kupatikana vibarua katika eneo la kufugia. Kuwepo kwa vibarua kutamsaidia mfugaji kuweza kutoa huduma zake kwa ufanisi kwa kuwa atakuwa na wasaidizi wa kutosha na hivyo kazi kama za utengenezaji wa chakula cha samaki, ulishaji na uvunaji hazitakuwa ngumu kwa mfugaji, cha msingi ni hao vibarua kuwa wanakaa karibu na eneo la kufugia ili kupunguza gharama za usafiri.
Kwa kuhitimisha hatua hii ya 1 ya sifa za eneo zuri la kufugia samaki inasisitizwa kuwa ni jambo muhimu kufanya uchaguzi mzuri na ulio sahihi wa eneo la kufugia ili kufanikisha kazi ya ufugaji wa samaki kwa urahisi na ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment