Mboga ni mmea au sehemu yoyote ya mmea inayoweza kuliwa na binadamu ambayo haina sukari kama
matunda. Mboga huweza kuliwa zikiwa zimepikwa na mara nyingi huwekewa chumvi ili kuongeza ladha na pia
huweza kuliwa zikiwa mbichi kwa mfano kwenye kachumbari. Mboga ni sehemu muhimu sana katika mlo
uliokamilika, hii imesababisha ukuaji wa kasi wa soko la mboga na upandaji wa mboga katika maeneo mengi
ya mijini na vijijini.
Sehemu za mmea ambazo zinaweza kutumika kama mboga
I. Majani
Mboga nyingi hutoka kwenye majani ya mimea. Mara nyingi haya majani huwa ya rangi ya kijani kwasababu
ya kutengeneza chakula cha mmea kutoka kwenye mionzi ya jua na huwa na virutubisho vingi muhimu katika
mwili wa binadamu kwa vile vitamin. Miongoni mwa majani ambayo huliwa kama mboga ni Kabichi, Spinach,
Chinese, Mchicha na figiri.
II. Mizizi
Mizizi ya baadhi ya mimea ni mboga nzuri na ina virutubisho kama vile vitamin A ambayo huimarisha macho
na kuongeza uwezo wa kuona. Miongoni mwa mizizi ambayo huliwa kama mboga ni karoti.
III. Tunda
Tunda kwa maana ya kibustani ni sehemu ya mmea ambayo hubeba mbegu na inalika ikiwa mbichi au
imepikwa. Mfano wa mimea ambayo sehemu ya tunda ni mboga ni kama vile nyanya, matango, bilinganya na
bamia.
IV. Bulb (Tunguu)
Hii ni sehemu ya mmea ambayo hukua chini ya ardhi kwa mfano vitunguu (maji na swaumu). Mboga za aina
hii ni muhimu sana katika mwili wa binadamu kwani husaidia kusafisha damu na huongeza ladha na harufu
nzuri katika chakula.
V. Tuber (Kiazi)
Hii ni aina ya mboga ambayo ni mzizi unaohifadhi chakula cha mmea. Aina hii ya mboga husaidia kujaza
tumbo na kufanya usihisi njaa haraka. Mfano wake ni viazi (mviringo na vitamu).
VI. Nyinginezo
Sehemu nyingine za mmea ambazo hutumika kama mboga ni pamoja na jicho la ua (cauliflower), mbegu
(kunde na maharage), shina (tangawizi), chipukizo/kimea (majani ya kunde, soybean).
Mfano wa mboga mboga
i) Bilinganya ii) kabichi iii) karoti iv) Mchicha
Umuhimu wa vyakula vya jamii ya mboga mboga mwilini
Watu hushauriwa kula vyakula vya jamii ya mboga mboga kwa wingi. Sababu kubwa ni kutokana na faida za
kiafya ambazo huletwa kutoka kwenye mboga mboga ambazo haziwezi kupatikana kutoka kwenye vyanzo
vingine. Mboga zina vitamins na madini (minerals) kama vile potassium, vitamin A & C hupatikana kwa wingi
kwenye mboga mboga na huhitajika mwilini kila siku ili kuusaidia kuwa na afya na kuweza kukinga au kuzuia
maradhi. Virutubisho vingine husaidia kukinga moyo na figo dhidi ya maradhi na huzuia kansa
Kanuni bora za ukuzaji wa mboga mboga
1. Kuchagua eneo
Katika kuchagua eneo kwaajili ya kupanda mboga ni muhimu kuzingatia vitu vifuatafvyo;
Mwinuko: Eneo lisiwe kwenye mwinuko mkali kwa sababu husababisha mmomonyoko wa udongo.
Endapo sehemu itakuwa na mwinuko, tengeneza makingamaji ili kuzuia mmomonyoko.
Udongo: Chagua udongo ambao una rotuba na wenye uwezo wa kupitisha maji kwa urahisi.
Chanzo cha maji: Eneo la Bustani liwe karibu na maji ya kudumu au chanzo cha maji ili kurahisisha
umwagiliaji na maji yasiwe na chumvi nyingi kwani huathiri ukuaji wa mimea.
Kitalu: Kisiwe mahali palipo na kivuli kingi kwani husababisha mimea kutokupata mwangaza wa jua na
kushindwa kutengeneza chakula hivyo kuwa dhaifu.
Kuzuia upepo mkali: Upepo mkali huharibu mimea, kuvunja majani na matawi na husafirisha vimelea
vya ugonjwa na wadudu. Eneo la Bustani lioteshwe miti mipakani ili kuzuia upepo mkali.
2. Kutayarisha shamba
Wakati wa kulima ni muhimu kukatua udongo katika kina cha kutosha, mabonge yalainishwe ili kurahisisha
upitaji wa maji na hewa katika udongo. Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya
maji yaweze kukaa kwenye udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi
ili kuzuia maji yasituame.
3. Kutumia mbegu bora
Mbegu bora ni zile zilizokomaa na kukauka vizuri, ambazo hazijashambuliwa na magonjwa au wadudu na
zenye uwezo wa kuota vizuri zikipandwa. Inashauriwa kununua mbegu kutoka kwa wakala halali.
4. Kuotesha na kupanda mboga
Kina cha kuotesha mbegu kinategemea na ukubwa wa mbegu yenyewe. Mbegu ndogo, hupandwa katika kina
kifupi zaidi kuliko mbegu kubwa. Baadhi ya mbegu huoteshwa kwanza kwenye kitalu kisha mche huhamishiwa
bustanini au shambani.
5. Kumwagilia maji
Hakikisha udongo una unyevu nyevu wa kutosha wakati wote na mmea unapata maji. Epuka kumwagilia maji
mengi sana kwani husababisha miche au mbegu kuoza.
6. Kuweka kivuli na matandazo
Utandazaji wa majani makavu na uwekaji wa kivuli ni muhimu ili kuzuia jua linaloweza kunyausha miche.
Matandazo huhifadhi unyevu, joto la udongo na hupunguza palizi ya mara kwa mara.
7. Matumizi ya mbolea
Mboga hustawi vizuri zaidi katika udongo uliowekwa samadi, mboji au mbolea vunde ya kutosha huwekwa
kwenye udongo kabla ya kupanda au kupandikiza mimea. Debe moja huhitajika kwenye tuta lenye upana wa
mita moja. Mbolea huuongezea mmea virutubisho na kuufanya ukue na kuzaa vizuri.
8. Kubadilisha mazao
Utaratibu huu ni ule wa kuacha kupanda mfululizo aina ile ile ya zao katika eneo moja. Inashauriwa kubadilisha
aina ya zao ili kusaidia kupunguza kuenea kwa magonjwa na wadudu na pia kuhifadhi rotuba ya udongo.
9. Matunzo mengineyo
Kupalilia na kukatia mimea pale inapohitajika ni muhimu sana kwani magugu hufanya mimea isikue vizuri kwa
kutumia virutubisho kutoka kwenye udongo.
10. Kuvuna
Mboga nyingi za majani hutakiwa kuvunwa kabla hazijakomaa sana. Baada ya kuvuna, inashauriwa kuweka
mboga kwenye eneo safi na salama ili kuweza kuzuia magonjwa yatokanayo na vyakula. Kumbuka kuosha mboga kabla ya kula au kupika.